SHUKRANI
Kazi hii imekamilika kutokana na michango ya watu mbalimbali walioshirikiana nami kuona inafanyika kama ilivyopangwa. Sina budi kutoa shukrani zangu za dhati kwa watu wote walionisaidia katika kufanikisha utafiti huu. Kwanza, kabisa napenda kumshukuru Mungu kwa kunipa uhai, uzima na afya njema hata nikaweza kufanikisha kazi hii bila matatizo yoyote yale ya kiafya. Pia alinipa akili na ufahamu wa kufanikisha kazi hii na kufikia tamati. Pili, namshukuru msimamizi wangu, Dkt Muhammed Seif Khatib ambaye amekuwa nami bega kwa bega ili kuhakikisha kazi hii inafikia kiwango hiki. Licha ya yeye kuwa na shughuli nyingi lakini alijitolea muda wake mwingi katika kunisahihisha na kunielekeza pale nilipohitaji msada. Nauthamini sana mchango wake. Mungu ambariki na amzidishie moyo wa imani. Tatu, naishukuru sana familia yangu akiwemo mke wangu mpenzi Ashura Ali na watoto wetu Nayfat Makame, Ummu Ayman Makame na Suhaila Makame kwa kunikubalia kujiunga na chuo bila kujali upweke walionao na kunisaidia pale nilipohitaji msaada wa hali na mali. Mungu awazidishie baraka na neema katika maisha yao. Nne, nawashukuru sana rafiki zangu na wanafunzi wenzangu ambao tulishirikiana na kushauriana vyema katika masomo akiwemo Rasuli Muhammed, Haruwa Kheir, Zuhura Said, Arafa Jumanne na Zeyana Omar, kwa pamoja nawatakia kila la kheri katika maisha yao. Tano, shukurani zangu za dhati kabisa ziwafikie „Ahlul dhikiri‟ wote wakiwemo Makhalifa, Muridi, Watu wazima na Walimu wa Madrasa kwa kunisaidia kupata data mbalimbali za utafiti wangu. Mungu awajaze neema. Mwisho shukurani zangu za pekee kabisa zimfikie mwalimu wangu Dkt. Muhyyidin Ahmad Khamis (maalim Siasa) mkuu wa chuo cha Kiislamu Zanzibar kwa kunisaidia kunipa mwongozo katika utafiti huu. Mungu amzidishie imani na neema katika maisha.