SHUKRANI
Shukrani jazila nazitakadamisha kwa Mwenyezi Mungu Raufu, imetimia tasnifu! Yeye ndiye wa kushukuriwa zaidi, amenipitisha salama katika tesi za ulimwengu katika kipindi chote cha masomo ya darasani na wakati wa uandishi wa tasnifu hii. Ama kwa hakika kidole kimoja hakivunji chawa, wala figa moja haliinjiki chungu, na mkono mmoja hauchinji ng‟ombe, walipata kusema wahenga. Kamwe siwezi kujidai kuwa yote nilofanya ili kazi hii itimie nimeyafanya kwa urazini ama ujanja wangu tu, ila ni kwa jamala na jitihada za watu mbalimbali walonipa misaada na ushirikiano wao azizi wakati wa mchakato wa kuandika tasnifu hii. Wote ninawatongolea nemsi zao sufufu. Mtima wangu unawiwa kuwataja wote kwa majina yao, lakini orodha yao ndeeeefu inabinywa na uchache wa karatasi. Lakini kwao wote ninasema, “Shukrani jazila.” Baada ya kumshukuru Rabuka kwa jamala ya uhai na vyote, sichelei kumtaja awali awaa msimamizi wangu, Prof. J.S. Madumulla. Huyu ni mwalimu ambaye nawiwa mfano madhubuti wa kumfananisha naye. Kwake nimejifunza mambo mengi mazuri kama mwalimu, kiongozi na mzazi. Hakika, yeye ni mfano wa kuigwa. Alinifaa sana kwa msaada wake adhimu na maelekezo yake aushi aliyonipatia katika kipindi chote cha utafiti wangu. Hata pale nilipohisi kukata tamaa, kutokana na changamoto mbalimbali zilizoniandama, alinitia moyo. Aliniamirisha na kunitia ashiki ya kusonga mbele na kwa hiyo, kwa mwongozo wake hakuna ambacho kilikwenda arijojo. Namshukuru kwa fikra na mawazo yake kuhusu mada yangu ya utafiti, amenifanya niwe mwanafunzi wa kwanza kutoka Tanzania kushughulikia utafiti kwa mkabala wa usemezano, baada ya Wakenya wachache walioanza. Kwake ninachoweza kusema, “Baba, sina cha kukulipa zaidi ya kusema, „asante.